Search This Blog

Thursday, April 12, 2012

NINI MAANA YA WOKOVU?

WOKOVU NI NANI?
           Wokovu ni mpango aliouandaa Mungu mwenyewe wa kumtafuta mwanadamu aliyepotea na kumleta awe chini ya milki yake. Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa;(Tito 2:11-12),  maandiko yanatuambia ya kuwa neema hii inatufundisha kukataa ubaya na tama za kidunia  au kwa maana nyingine hii neema imekuja ili tuache  uovu au tuache dhambi na baada ya kuziicha dhambi tuishi maisha ya kiasi, na haki, na utauwa (utakatifu). Biblia inaposema hii neema ni kwa ajili ya wanadamu wote in maana ya kuwa haikutoka kwa mwanadamu awaye yote bali ilitoka kwa Mungu mwenyewe na kwa kuwa inatoka kwa Mungu basi ujue inamgusa kila mwanadamu na ndani yake imejaa mafundisho ya kutuelekeza ni kwa namna gani tunaweza kuishi katika ulimwengu huu wa sasa na si ule ujao bali ulimwengu huu wa sasa; na hapa ndipo tunapopata jibu kuwa kuokoka ni hapa duniani na sio mbinguni.

Wokovu sio dini  kama wengine wanavyodhani, wala sio dhehebu fulani wala ubatizo fulani bali wokovu ni mpango unaotoka kwa Mungu mwenyewe na lazima uendane na kuacha na kuchukia uovu na kuamua kuishi maisha mengine tofauti na ambayo ulikuwa unaishi awali na hayo maisha yawe yanaratibiwa na Roho Mtakatifu kila siku.

Tunaposema ni neema ya Mungu maana yake, Mungu huitoa bure pasipo malipo wala gharama zozote bali yeye mwenyewe Mungu amekwisha kulipa gharama zote. (Free of cost)

NINI MAANA YA KUOKOKA.
            Kuna maana mbalimbali au tafsiri nyingi juu ya kuokoka ila na tuangalie maana chache katika maandiko jinsi yasemavyo.

      Kuokoka ni kuzaliwa mara ya pili. (Yohana 3:1-6), mstari wa 3 unasema hivi; Yesu akajibu, akamwambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu. Na mstari wa 6 wa Yohana 3 unasema; Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili; na kilichozaliwa kwa Roho ni roho. Kinachofanyika baada ya mtu kumkubali Kristo maishani mwake Roho Mtakatifu anamzaa tena huyu mtu kwa jinsi ya roho haijalishi ni mtu mzima au mtoto; badiliko linatokea  rohoni ambalo halionekani kwa jinsi ya mwili. Ndani mwako unafanyika kiumbe kipya (2 Kor 5:17) utu wako wa kale ulionao unavuliwa na Roho Mtakatifu na unavikwa utu upya na ndiyo maana maandiko yanasema ya kuwa unazaliwa kwa maraya pili.
  Maana nyingine ni; Kuamini na kukiri ya kuwa Yesu ni Bwana na kuishi kama ulinyokiri. (Rum 10:9-10), Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu. Kuokoka lazima kuendane na kukiri kwa kinywa na kuamini ndani ya moyo juu ya Yesu Kristo na maisha yako yaendane kama ulivyokiri na kuamini, hili ni jambo muhimu sana katiaka maisha ya mtu aliyeokoka , wapo walokole wengi sana leo ambao wanamuaibisha Yesu kwa sababu wanaishi kinyume na walivyokiri na ni jambo ambalo linamuhuzunisha Mungu sana. Kwa mfano; mtu anaweza kuwa ameokoka lakini bado ni mzinzi, mwasherati, msengenyaji na nk. Mungu na atusaidie sana!! Amen.

TOFAUTI KATI YA DINI NA WOKOVU
            Dini ni mpango wa mwanadamu wa kumtafuta na kumwabudu Mungu, inaweza kuwa ni Mungu aliye hai (The Most High) au miungu. (gods), {Kutoka 32:1-8}…wamejifanyizia ndama ya kuyeyusha wakaiabudu na kuitolea dhabihu, wakasema, Hiyo ndiyo miungu yako, Ee Israeli, iliyokutoa katika nchi ya Misri. Hii ina maana mwanadamu akikosa cha kuabudu ataabudu chochote alichokichagua kuwa mungu wake.

Jambo ambalo nataka ulielewe mpendwa katika Kristo ni kwamba hakuna hata dini moja duniani ambayo inaweza kumfikisha mwanadamu mbinguni ila YESU peke yake ndiye awezaye kufikisha mwanadamu kwenye uzima wa milele. Mungu anatuhitaji kuuthamini wokovu maana Yesu alipokuja duniani alizikuta dini na aliziacha dini; alichokihitaji Yesu hadi leo ni wote wenye mwili wamuamini yeye peke yake ili aweze kuwaokoka na kuwapa uzima wa milele.

            Wokovu kama tulivyoona awali, ni mpango wa Mungu mwenyewe wa kumtafuta mwanadamu aliyepotea (katika dhambi) na kumfanya awe chini ya milki/utawala au chini ya utaratibu/mfumo wake. (Tito 2:11-12).

FAIDA ZA KUOKOKA
             Zipo faida nyingi sana ambazo mtu aliyeokoka anatakiwa kuzipata wakati akiendelea kumtukuza Mungu hapa duniani, hizi nilizokuandikia hapa ni chache kati ya nyingi. Roho Mtakatifu ataendelea kukufundisha njia nyingine kadri unavyoendelea kukua kiroho. 

  Tunasamehewa dhambi zote.
                        Mdo 10:43                   Isaya 44:22
                        Zab 103:12                  Isaya 43:25

     Tunafanyika wana wa Mungu.
Yoh 1:12                     Rum 8:15-16
                       
     Tunapata uzima wa milele
1 Yoh 5:13                  Yoh 20:31


     Roho Mtakatifu anakaa ndani yetu.
1 Kor 3:16-17              2 Kor 6:16
1 Kor 6:19-20              Rum 8:9-10

      Tunavikwa utu upya.
2 Kor 5:17                   Efeso 4:22-24

   Yesu anafanya makao kwetu.
Ufunuo 3:20                Yoh 15:14-15

NITAJUAJE KAMA NIMEOKOKA?
            Inawezekana umewahi kukutana na swali la namna hii au umewahi kusikia watu wakiulizwa swali kama hili ya kwamba ni kitu gani kinachomfanya mtu ajue ya kuwa ameokoka je, ingekuwa wewe leo unaulizwa swali la jinsi hii ungejibuje? Hebu tuangalie maandiko yanasemaje.

 (Rum 8:16), Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu; hii ni sababu mojawapo inayotupa uhakika ndani yetu ya kuwa sisi tumeokoka maana Roho Mtakatifu aliye ndani yetu anatushuhudia ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu, ambao ndani yetu hakuna tena hukumu y dhambi inayotushaki ya kuwa sisi tu watenda dhambi wala hakuna hofu ya jehanamu kwa sababu watoto wa Mungu kwao ni mbinguni na si jehanamu.

  Sababu ya pili tunaipata katika kitabu cha waraka wa kwanza wa Yohana, sura ya tano na mstari wa kumi na tatu (1 Yohana 5:13), Nimewaandikia ninyi mambo hayo, ili mjue ya kuwa mna uzima wa milele, ninyi mnaoliamini Jina la Mwana wa Mungu. Maandiko yanena wazi ya kuwa uzima wa milele unakaa ndani yetu sisi tulioliamini jina la Yesu Kristo; uzima wa milele maana yake ni maisha ya milele (eternal life)  yapo kwa waliookoka, Yesu ndiye atupaye huo uzima wa milele pamoja na Roho Mtakatifu aliye ndani yetu. Haleluya!




JE, NISIPOOKOKA NITAFIKA MBINGUNI?
           Jibu ni rahisi sana, hapana huwezi kufika mbinguni, kwa sababu:-

           (Yohana 3:18), Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu. Biblia inasema wazi hata kama ungali hai leo lakini kama hujamwamini Yesu Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yako; umekwisha kuhukumiwa tayari hata kama siku ya hukumu haijafika, na ikitokea ukifa leo kama bado hujamwamini Yesu Kristo huwezi kwenda mbinguni.

  Yesu akamwambia, mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi. (Yoh 14:6), kuna mambo matatu hapa maandiko yanataja sifa au uwezo alionao Yesu, anasema yeye ni njia, kweli, na uzima; hatuwezi kumfikia Mungu wala kumuona kwa namna yoyote ile isipokuwa Yesu Kristo mwenyewe ametupa  kibali cha kufika mbele za Mungu. Amen! Amen!.

N
atumaini ndugu mpendwa umepata msaada wa kukusaidia juu ya somo hili, ni maombi yangu kwako Mungu azidi kuweka ndani yako roho ya kupenda kujifunza ili uzidi kukua katika kumwishia yeye siku zote za maisha yako.
Usisite kuniandikia au kunipigia simu pale ambapo utakuwa una maswali au una hitaji tumuombe Mungu kwa pamoja katia jambo ambalo umekutana nalo na kwako limekupa ni tatizo, maana sisi tu viungo vya Kristo tukitegemeana kila kimoja na chenzake ili kwa pamoja tuweze kuujenga mwili wa Kristo.
Na Mungu wangu akubariki sana unapokwenda kuyaweka kwenye matendo yale ambayo Roho Mtakatifu amekufundisha katika somo hili, sifa na heshima ni za kwake kwa maana anastahili.  


                                   


6 comments: